
HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE,
Mheshimiwa Samuel Sitta, Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba;
Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar;
Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Mheshimiwa Anne Semamba Makinda; Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano;
Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho, Spika wa Baraza la Wawakilishi na Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalum la Katiba ;
Mheshimiwa Rashid Othman Chande, Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Othman Makungu, Jaji Mkuu wa Zanzibar;
Viongozi Wakuu Wastaafu;
Waheshimiwa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba;
Waheshimiwa Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba;
Wageni waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Pongezi
Nakushukuru sana Mheshimiwa Mwenyekiti kwa kunipa
fursa ya kuja kuzungumza na Waheshimiwa Wajumbe wa Bunge letu Maalum la
Katiba katika siku hii muhimu na ya kihistoria kwa nchi yetu. Nimekuja
kuwatakia heri na naungana na Watanzania wenzetu wote kuwaombea baraka
za Mwenyezi Mungu, ili muweze kuifanya kazi yenu kwa utulivu, hekima,
umakini mkubwa na kuimaliza kwa salama na kwa mafanikio yanayoyatarajiwa
na Watanzania.
Natoa pongezi nyingi kwako na kwa Makamu wako kwa
kuchaguliwa kwenu kuongoza Bunge hili maalumu na la kihistoria. Ushindi
mkubwa mliopata ni kielelezo tosha cha imani kubwa na matumaini
waliyonayo Wajumbe wenzenu kwenu. Matumaini yao ndiyo matumaini ya
Watanzania wote, kwamba mtaliongoza vizuri Bunge hili, ili liweze
kutimiza kwa ufanisi mkubwa jukumu lake muhimu sana katika historia ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Niruhusu pia niwapongeze kwa dhati Wajumbe wote wa
Bunge Maalum la Katiba kwa bahati ya aina yake waliyopata ya kutunga
Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Fursa hii hutokea mara
chache sana katika historia ya nchi yo yote na watu wake. Mkifanikiwa
kuipatia nchi yetu Katiba nzuri majina yenu yataandikwa kwa wino wa
dhahabu, katika kumbukumbu za historia ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Ni matarajio ya Watanzania kuwa mtatunga Katiba
itakayokubalika na wengi. Katiba inayotekelezeka. Katiba itakayoimarisha
Muungano wetu kwa kuondoa changamoto zilizopo sasa. Katiba itakayoipa
nchi yetu mfumo bora wa kuongoza na kuendesha mambo yetu. Katiba
itakayoimarisha umoja, upendo, ushirikiano na mshikamano miongoni mwa
wananchi wa Tanzania, licha ya tofauti zao za asili za upande wa
Muungano na maeneo watokako, au tofauti za jinsia, rangi, kabila, dini
na ufuasi wa vyama vya siasa. Katiba itakayodumisha amani, usalama na
utulivu nchini. Katiba itakayostawisha zaidi demokrasia, haki za
binadamu, utawala wa sheria, utawala bora na kudhibiti maovu. Na, mwisho
ingawaje siyo mwisho kwa umuhimu, Katiba itakayoweka mazingira mazuri
kwa uchumi wa nchi kukua, na wananchi wengi kunufaika sawia na maendeleo
yatayopatikana.
Historia ya Katiba Nchini
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wajumbe;
Hii itakuwa mara ya tatu tangu kuzaliwa kwa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Aprili 26, 1964, kwa nchi yetu kuwa na mchakato
wa kutunga Katiba mpya. Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1965 ilipotungwa
Katiba ya Muda na mara ya pili ni mwaka 1977 ilipotungwa Katiba ya
Kudumu tuliyonao sasa. Tofauti na mara mbili zilizopita, safari hii
mchakato unahusisha watu wengi zaidi. Wananchi wameshiriki moja kwa moja
kutoa maoni yao kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, na ndio watakaofanya
uamuzi wa mwisho kuhusu Katiba mpya kwa kura ya maoni. Wananchi pia
walipata nafasi ya kuchagua Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya
yaliyojadili Rasimu ya Kwanza ya Katiba. Pia walipata nafasi ya kutoa
maoni yao kupitia Mabaraza ya Katiba ya taasisi. Katika Bunge hili wapo
wananchi 201 kutoka makundi mbalimbali.
Katika mchakato wa kutunga Katiba za mwaka 1965 na
1977 kulikuwapo Tume za Kuandaa Rasimu na Bunge Maalum la Katiba kama
ilivyo katika mchakato huu. Hata hivyo, kwa Katiba zilizopita Wabunge wa
Bunge la Jamhuri ya Muungano pekee ndio waliounda Bunge Maalum. Safari
hii Bunge Maalum linajumuisha Wabunge, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi
na wananchi 201 wanaotoka kwenye jamii, wakiwakilisha asasi na makundi
mbalimbali ya Watanzania kutoka Zanzibar na Tanzania Bara. Mchakato wa
sasa utaishia kwenye kura ya maoni itakayoshirikisha wananchi wote wa
Tanzania wanaoruhusiwa kupiga kura. Michakato iliyopita iliishia Bunge
Maalum pekee.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tangu kutungwa kwake, tarehe 25 Aprili, 1977, mpaka
sasa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 imefanyiwa mabadiliko
takriban mara 14. Mabadiliko hayo yalitokana na kufanyika au kutokea kwa
mabadiliko muhimu ya kiuchumi, kisiasa na kijamii katika nyakati
mbalimbali hapa nchini na katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kwa ruksa yako naomba nitaje baadhi ya mabadiliko yaliyofanywa:-
-
Mabadiliko ya 1979 yaliunda Mahakama ya Rufani ya Tanzania kufuatia kufa kwa Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977.
-
Mabadiliko ya mwaka 1980 yalifanyika baada ya kutungwa kwa Katiba ya Zanzibar, hivyo kulazimu Katiba hiyo kutambulika kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
-
Mabadiliko ya mwaka 1984 yaliweka utaratibu wa ukomo wa vipindi vya Urais ambao haukuwepo kabla ya hapo. Aidha, masuala ya Haki za Binadamu (Bill of Rights) yaliingizwa kwa mara ya kwanza katika Katiba. Vilevile, Mahakama ya Rufani ya Tanzania na mambo mengine ya iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki yaliongezwa katika Orodha ya Mambo ya Muungano.
-
Mwaka 1992, yalifanyika mabadiliko yaliyoanzisha Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa badala ya ule wa Chama kimoja uliokuwepo tangu 1965. Pia utaratibu wa uchaguzi wa Rais na Wabunge ulirekebishwa ili uendane na mfumo wa vyama vingi vya siasa. Vilevile utaratibu wa kuwa na viti maalum vya wanawake katika Bunge ulianzishwa. Wakati ule ilikuwa asilimia 15 ya Wabunge wote. Aidha, kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu Bunge lilipewa mamlaka ya kumwajibisha Rais na Waziri Mkuu kupitia kura ya kutokuwa na imani.
-
Mabadiliko ya mwaka 1994 yaliweka mfumo mpya wa kumpata Makamu wa Rais kupitia Mgombea Mwenza.
-
Mwaka 2000 na 2005, pamoja na mambo mengine yalifanyika mabadiliko yaliyopanua wigo wa Haki za Binadamu na kuongeza uwakilishi wa wanawake.
Umuhimu wa Mabadiliko ya Katiba
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kufanyika kwa mabadiliko hayo kunathibitisha utayari
wa Serikali kufanya mabadiliko kila ilipoonekana inafaa kufanya hivyo.
Pamoja na kufanya yote hayo na Serikali kuwa na msimamo huo, kumekuwepo
na madai yaliyokuwa yanajirudia ya kutaka Katiba ya Tanzania iandikwe
upya. Wako watu walioimithilisha Katiba yetu na nguo yenye viraka vingi
mno kiasi kwamba ingefaa kununua mpya badala ya kuendelea kuivaa.
Madai ya kutaka Katiba mpya yalipazwa sauti baada ya
kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa. Wapo waliokuwa wanadai Katiba
mpya kwa imani, eti kwamba, itawawezesha kuishinda CCM. Lakini, si hayo
tu, hata katika mchakato wa Serikali zetu mbili kushughulikia kero za
Muungano, imedhihirika kuwa baadhi ya changamoto zilikuwa zinahitaji
mabadiliko ya Katiba ili kuzipatia ufumbuzi wa uhakika na wa kudumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa kutambua ukweli huo na baada ya kushauriana na
kukubaliana na viongozi wenzangu wakuu wa Chama tawala na Serikali zetu
mbili wakati ule, ndipo tarehe 31 Desemba, 2010, nikatangaza dhamira ya
kuanzisha mchakato wa kutunga Katiba mpya. Nilieleza siku ile kuwa
katika mchakato huo tutakuwa na ushirikishwaji mpana wa wananchi wa
Tanzania kwa makundi yao ya jinsia, dini, siasa na shughuli wazifanyazo
kujipatia riziki na kwa maeneo wanayotoka katika pande zetu mbili za
Muungano.
Mchakato wa Katiba Mpya
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tarehe 16 Machi, 2011 Baraza la Mawaziri liliridhia
kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya kuliongoza taifa katika
mchakato wa kutunga Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Tarehe 18 Novemba, 2011 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
lilipitisha Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Kwa mujibu wa
Sheria hiyo, mchakato wa kutunga Katiba Mpya ulikuwa unaanza kwa kuunda
Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Tume hiyo imepewa jukumu la kusikiliza
maoni ya wananchi mmoja mmoja na kwa makundi yao ya maslahi, taasisi zao
na kupitia Mabaraza ya Katiba. Mwishowe Tume imetakiwa kutengeneza
Rasimu ya Katiba mpya itakayofikishwa kwenye Bunge Maalum la Katiba
kujadiliwa na Katiba mpya kutungwa. Mchakato wa Katiba utahitimishwa kwa
wananchi kupiga kura ya maoni ya kuamua kama wanaikubali au kuikataa
Katiba mpya.
Tarehe 6 Aprili, 2012 nilifanya uteuzi wa Wajumbe wa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kuwaapisha tarehe 13 Aprili, 2012. Tume
ilianza kazi tarehe 2 Mei, 2012 na kuikamilisha kwa mafanikio, hatua
zote zilizoihusu na kukabidhi kwangu na kwa Rais wa Zanzibar, Taarifa ya
Tume na Rasimu ya Katiba tarehe 30 Desemba, 2013. Kitendo cha
Mwenyekiti wa Tume, Mheshimiwa Joseph Warioba kuwasilisha Rasimu hiyo
mbele ya Bunge hili tukufu tarehe 18 Machi, 2014, kinahitimisha rasmi
kazi ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Kazi inayofuatia ni ya Bunge hili
kujadili, kuamua na kutunga Katiba mpya. Baada ya hapo Katiba mpya
itafikishwa kwa wananchi kwa uamuzi wa mwisho kwa njia ya kupiga kura ya
NDIYO au HAPANA.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Rasimu ya Katiba ilichapishwa kwenye gazeti la
Serikali na magazeti mengine yanayosomwa na wananchi kama ilivyoagizwa
katika Kifungu cha 20(2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Pamoja na
hayo, Taarifa ya Tume na Rasimu ya Katiba viliwekwa wazi kwenye tovuti
ya Tume kwa kila mtu kusoma. Inafurahisha kuona kuwa watu wengi
wameisoma Taarifa ya Tume na Rasimu ya Katiba na kumekuwa na mjadala
mpana kuhusu nyaraka zote hizo muhimu. Watu wengi wametoa maoni yao na
wanaendelea kufanya hivyo. Kwa maoni yangu hili ni jambo jema sana na ni
kielelezo thabiti kuwa demokrasia imestawi na inazidi kuota mizizi
Tanzania. Pia, kwamba, Watanzania wako huru kushiriki na kutoa maoni yao
kwa mambo yanayowahusu.
Pongezi kwa Tume
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa mara nyingine tena narudia kutoa pongezi za dhati
kwa Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya uongozi wa
Mheshimiwa Jaji Joseph Warioba akisaidiwa na Mheshimiwa Jaji Augustino
Ramadhani, kwa kazi kubwa na nzuri waliyofanya. Kazi yao haikuwa rahisi
hasa ukizingatia ukubwa wa nchi yetu, wingi wa watu wake, utitiri wa
taasisi na pigo la kumpoteza Mjumbe mwenzao muhimu Dkt. Sengondo Mvungi
aliyetangulia mbele ya haki katikati ya mchakato.
Pamoja na hayo, kwa bidii kubwa Wajumbe wa Tume wameweza kutembelea mikoa yote nchini na kuwafikia watu 351,644 waliotoa maoni yao kwa mdomo na kwa maandishi. Halikadhalika, walipokea na kuchambua maoni 772,211
kutoka kwa wananchi na taasisi mbalimbali. Baada ya kupokea maoni ya
wananchi, kufanya utafiti na kwa kutumia maarifa na uzoefu wao, Wajumbe
wakafanya kazi ngumu, kuliko yote, ya kutengeneza Rasimu ya Katiba
iliyoko mbele ya Bunge hili. Ni kweli kwamba Wajumbe hawakuweza
kuwafikia wananchi wote wa Tanzania, lakini wameweza kuwafikia wananchi
wengi, ambao kwa kiasi kikubwa wanawakilisha taswira na mitazamo mipana
ya jamii yetu.
Baadhi ya Masuala Yaliyojitokeza Katika Mjadala wa Mapendekezo ya Tume
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tume imefanya kazi nzuri, yenye thamani kubwa na ya
manufaa kwa taifa la Tanzania. Rasimu imeandikwa vizuri na kwa weledi wa
hali juu. Tume imetoa mapendekezo ambayo kwa kiasi kikubwa yanahuisha
na kuboresha Katiba ya nchi yetu, kwa namna ya pekee. Katiba
inayopendekezwa, imejumuisha dhana na mambo kadhaa mapya yanayokwenda
vyema na wakati tulionao na kuweka msingi mzuri kwa huko mbele tuendako.
Kwa taratibu za kawaida za marekebisho ya Katiba tuliyonayo, isingekuwa
rahisi kuingiza mambo mengi mapya kiasi hiki.
Wajumbe Wana Kazi Kubwa
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Waheshimiwa Wajumbe;
Rasimu ya Katiba ni kitabu kikubwa kilichosheheni mambo mengi. Kina kurasa 106, sura 17 na ibara 271.
Wajumbe wa Bunge hili mnatakiwa kusoma na kuelewa vizuri kila
kilichoandikwa ili muweze kufanya uamuzi ulio sahihi. Mnawajibika
kuchambua kwa kina na umakini mkubwa kila kilichomo, sura kwa sura,
ibara kwa ibara, sentensi kwa sentensi na hata neno kwa neno. Hamna budi
kujiridhisha kuhusu uandishi wa vifungu vya Rasimu ya Katiba na kufaa
kwa dhana mbalimbali zilizoingizwa na kujengeka katika Rasimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kile ambacho Wajumbe mtaona kinastahili kuboreshwa au
kurekebishwa au kufutwa msisite kufanya hivyo ili Watanzania wapate
Katiba iliyo bora. Msipofanya hivyo kuna hatari ya kupata Katiba ambayo
ni ngumu kuitekeleza. Aidha, tunaweza kuwa na Katiba ambayo
itanung’unikiwa na watu wengi na kusababisha madai ya kutaka ifanyiwe
marekebisho muda mfupi baada ya kupitishwa. Bunge hili linao wajibu
maalum wa kuzuia balaa hilo lisitokee katika nchi yetu. Ngazi mbalimbali
zilizowekwa katika mchakato huu ni kama chujio la kuepusha hali hiyo
isitokee. Kile ambacho hakikuonekana katika hatua moja kitaonekana
katika hatua inayofuata na kurekebishwa. Nawaomba fursa mliyonayo
muitumie vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Nimekwishaeleza kuwa moja ya jambo mnalotegemewa
kufanya ninyi wenzetu mliopewa dhamana ya kutunga Katiba ya nchi yetu ni
kujiridhisha na uandishi wake. Yapo maoni yaliyotolewa kuhusu uandishi
ambayo naomba myatafakari na kuamua ipasavyo. Kwa mfano, kuna baadhi ya
vifungu vya Katiba vinayopendekezwa vimekuwa na mambo mengi mno kuliko
inavyostahili Katiba kuwa (too prescriptive). Pia kuna mawazo
kwamba baadhi ya mambo hayangetakiwa kuwa katika Katiba bali yawe kwenye
Sheria zinazotafsiri utekelezaji wa Katiba yenyewe.
Yako mambo yaliyotajwa kwenye Katiba ambayo yanatakiwa kuelezwa wazi kuwa mtu hatakwenda mahakamani kuidai Serikali impatie (non justiciable).
Mambo yaliyotajwa kwenye Katiba ni mazuri na yanavutia, lakini lazima
yaendane na uwezo wa nchi na uchumi wake kuhimili. Simaanishi kwamba
tuyatoe kwenye Katiba, bali yabakie kama dhamira pale uwezo wa nchi
utakaporuhusu yatekelezwe. Tusipofanya hivyo, kuna hatari ya Serikali
kujikuta inalaumiwa au hata kufikishwa mahakamani kila wakati kwa madai
ya jambo moja au jingine ambayo haina uwezo nayo. Ni muhimu sana mambo
kama hayo muyatazame ili tusije kuwa na Katiba ambayo ni ngumu
kutekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Yapo pia maoni kuwa baadhi ya vifungu vina upungufu
katika uandishi wake, hivyo kuhitaji kufanyiwa marekebisho. Isipofanyika
hivyo kunaweza kuwepo athari na nyingine zinaweza kuwa mbaya. Kwa
mfano, Ibara ya 2 ya Rasimu inayotambulisha eneo na mipaka ya nchi yetu.
Ibara hiyo inasomeka kuwa “Eneo la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ni eneo lote la Tanganyika likijumuisha sehemu yake ya bahari
na eneo lote la Zanzibar likijumuisha sehemu yake ya bahari”.
Maelezo hayo yameacha kutambua, kwa upande wa
Tanzania Bara, sehemu yetu ya maziwa na mito ambayo ni kubwa sana. Kwa
nini tuache kuitaja? Je hatutoi nafasi kwa nchi tunazopakana nazo siku
moja wakaja kupora sehemu zetu hizo na sisi kukosa utetezi kwa kuwa hata
Katiba yetu haikuyatambua maeneo hayo kuwa ni yetu? Hili ni jambo kubwa
ambalo Bunge hili lazima mlirekebishe. Wakati ndiyo huu hakuna
mwingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Jambo jingine kuhusu uandishi ni mgongano kati ya
pendekezo la msingi la Tume la kuwa na muundo wa Serikali tatu na
majukumu ya Serikali ya Muungano ambayo kimsingi ni majukumu ya Serikali
za nchi washirika. Katika Rasimu hii malengo ya taifa yameainishwa na
Serikali ya Muungano inatakiwa kuhakikisha kuwa malengo hayo
yanatekelezwa na itoe taarifa Bungeni. Katika mfumo wa Serikali tatu
unaopendekezwa na Tume masuala yahusuyo uchumi na maendeleo ya jamii
kama vile kukuza kilimo, ufugaji, uvuvi, viwanda, biashara, pembejeo,
elimu, hifadhi ya jamii na kadhalika yako chini ya mamlaka ya Serikali
za nchi washirika. Mamlaka ya Serikali ya Muungano ni kwa mambo saba tu
yafuatayo:- Katiba na Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano, Ulinzi na Usalama
wa Jamhuri ya Muungano, Uraia na Uhamiaji, Sarafu na Benki Kuu, Mambo ya
Nje, Usajili wa Vyama vya Siasa, Ushuru wa Bidhaa na Mapato yasiyo ya
kodi yatokanayo na Mambo ya Muungano.
Kwa Rasimu kupendekeza muundo wa Serikali tatu na
kuipa Serikali ya Muungano majukumu ambayo haina mamlaka nayo, ni
kuzusha utata na migongano kati ya Serikali ya Muungano na nchi
washirika. Mkichagua mfumo wa Serikali tatu, inawalazimu muyaondoe mambo
hayo kwani Serikali ya Muungano haistahili kuyatekeleza na wala haina
uwezo wa kuweka masharti kwa Serikali za nchi washirika kwa mambo yaliyo
kwenye mamlaka ya nchi hizo. Lakini kama mtaamua tuendelee na muundo wa
Serikali mbili, mambo haya mazuri yanatekelezeka na Serikali ya
Muungano bila ya matatizo. Katika uandishi wa Rasimu Utumishi katika
Serikali ya Muungano haumo katika Orodha ya Mambo ya Muungano. Ni lazima
liwemo. Hayo ni baadhi tu ya masuala yahusuyo uandishi katika Rasimu.
Naamini mkiisoma Rasimu kwa makini mnaweza kuyagundua mengineyo.
Dhana Mpya
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Katika Rasimu kuna dhana mpya na mambo mapya kadhaa
yaliyoingizwa ambayo yanabadili utaratibu wa sasa wa uendeshaji wa nchi
na mambo mbalimbali. Nawaomba mfanye uchambuzi wa kina kwa kila
kinachopendekezwa na kujiridhisha kuhusu kufaa kwake na manufaa yake.
Fanyeni hivyo ili tujihakikishie kuwepo kwa mambo mazuri na uendeshaji
mzuri wa shughuli katika taifa letu changa.
Mambo ni mengi na kwa ufinyu wa muda sitaweza
kuyazungumzia yote. Niruhusuni nizungumzie baadhi ya dhana na mambo
mapya yaliyomo katika Rasimu. Jambo la kwanza, kwa mfano, linahusu Ibara
ya 128 (2)(d) inayoleta dhana ya “Mbunge kupoteza Ubunge iwapo
atashindwa kufanya kazi za Mbunge kwa miezi sita mfululizo kutokana na
maradhi au kizuizi ndani ya gereza”. Watu hawana tatizo na Mbunge kuwa
kizuizini ndani ya gereza kama amepatikana na hatia Mahakamani na
kuhukumiwa kifungo. Lakini, isijekuwa yuko rumande kwa tuhuma akisubiri
kesi kusikilizwa. Je akija kuonekana hana hatia na kuachiliwa? Naungana
na wale wanaoshauri kuwa jambo hili lifafanuliwe vizuri na kutambua
Mbunge kutiwa hatiani na kupata adhabu ya kifungo cha kipindi hicho. Ni
bora ifanyike hivyo sasa ili kuondoa mikanganyiko. Hakuna haja ya
kusubiri mpaka jambo hili lije kufafanuliwa baadaye kwa Sheria
itakayotungwa na Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa upande wa mtu kupoteza Ubunge kwa sababu ya “kuugua kwa miezi sita mfululizo”
ni maoni ya watu wengi kuwa huu ni ukatili ambao haustahili kufanywa na
Katiba. Kuugua ndiyo ubinadamu na wakati mwingine Mbunge anaweza kupata
ajali akiwatumikia wananchi wa Jimbo lake. Anaweza kuugua kwa miezi
sita au zaidi na kupona kabla ya kipindi chake cha Ubunge kufika mwisho.
Kwa nini awekewe ukomo wa miezi sita? Katiba ya mwaka 1977 tunayotumia
sasa haina sharti hilo. Watu wanauliza hoja na haja ya kuwa na sharti
hili kwenye Katiba mpya ni ipi? Wanasema kwa kweli anachostahili Mbunge
huyu kufanyiwa ni kuuguzwa afya yake iimarike ili aendelee kutumikia
watu wake, na siyo kupoteza uongozi wake. Tusiwatie watu kishawishi cha
kukatiza matibabu ili kukwepa sharti hilo. Ni vyema jambo hili
mkalitazama kwa makini, na muone kama linastahili kuwepo au hapana.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Katika Rasimu hii imeingizwa dhana mpya ya kuweka
ukomo wa vipindi vitatu kwa Wabunge. Tena mapendekezo haya hayasemi
vipindi vitatu mfululizo au la!. Jambo hilo limezua mjadala motomoto
katika jamii. Ni vizuri mkajiridhisha juu ya sababu za msingi na manufaa
ya kufanya hivyo hapa Tanzania. Mazoea yetu na ya kwingineko duniani ni
kuweka ukomo kwa Wakuu wa Nchi kwa sababu nzuri na rahisi kuzielezea.
Lakini, kuwawekea ukomo Wabunge ni jambo jipya na huenda Tanzania tukawa
wa kwanza. Nashawishika kuungana na wale wanaopendekeza kuwa pengine ni
mapema mno kuanzisha utaratibu huo hapa kwetu. Nachelea kuwa tutainyima
nchi yetu fursa ya kupata watu wenye maarifa na uzoefu mzuri wa uongozi
kwa nafasi ya Ubunge au kwa nafasi za uongozi wa Taifa bila ya sababu
za msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Jambo lingine jipya linalopendekezwa na Tume ni
utaratibu wa kumuondoa Mbunge katikati ya kipindi chake cha uongozi. Kwa
hoja linaonekana kuwa jambo jema lakini naomba athari zake mzitafakari
vizuri. Kuna hatari ya kuanzisha misuguano kwenye Majimbo na kuwaacha
Wabunge wasifanye kazi zao kwa utulivu bali wawe wanajihami dhidi ya
wapinzani wao kuwatengenezea fitna za kuwatoa. Utaratibu unaopendekezwa
wa Chama chake kujaza nafasi ya Mbunge inapokuwa wazi katika mazingira
hayo nao unaweza kuwa ndicho kichocheo kikubwa cha vuguvugu la kumuondoa
Mbunge. Walioshindwa kwenye kura ya maoni wanaweza kufanya kazi ya
kuwachimba wenzao mpaka waondoke. Jipeni muda wa kupima faida na hasa
thamani inayoongezwa na kuanzisha utaratibu huo. Naomba tujiridhishe
kama jambo hili jipya lina tija. Hivi kupewa nafasi kila miaka mitano
kurudi kwa wananchi hakutoshi kumuondoa Mbunge ambaye watu wamemchoka?
Muundo wa Muungano
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Jambo lingine kubwa lililopendekezwa na Tume ambalo
limevuta hisia za karibu watu wote nchini linahusu muundo wa Muungano
wetu kuwa wa Serikali tatu badala ya mbili za sasa. Pendekezo hili
limezua mjadala mkubwa tangu lilipotolewa katika Rasimu ya kwanza na
kurudiwa katika Rasimu ya pili. Wakati mwingine mjadala umekuwa mkali na
wa hisia kali kwa kila upande.
Kwa kweli hili ndilo jambo kubwa kuliko yote katika
Rasimu kwa sababu linapendekeza kuanzishwa kwa muundo na mfumo mpya wa
kuendesha nchi yetu. Hii ndiyo agenda mama ya Bunge hili ambayo kila
Mtanzania anasubiri kwa hamu uamuzi wenu utakuwa upi. Ombi langu kwenu
ni kuwa watulivu mnapojadili suala hili. Epukeni jazba ili mfanye uamuzi
ulio sahihi. Lazima mtambue uamuzi usiokuwa sahihi kwa jambo hili una
hasara kubwa. Tunaweza kupoteza kitu tulichokijenga kwa gharama kubwa
kwa nusu karne iliyopita. Tanzania inaweza kuwa nchi iliyojaa migogoro
na matatizo mengi ambayo hatunayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wajumbe;
Kama alivyoeleza Mwenyekiti wa Tume Mheshimiwa Jaji
Joseph Sinde Warioba, mara kadhaa, mjadala au madai ya kutaka muundo wa
Serikali tatu si jambo jipya. Ulikuwepo hata wakati wa mazungumzo ya
kuunganisha nchi zetu mbili mwaka 1964. Ulikuwa kiini cha kuchafuka kwa
hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar mwaka 1984. Muundo huu uliwahi
kupendekezwa na Tume ya Nyalali mwaka 1992, ndiyo hoja ya G55 mwaka 1993
na umependekezwa pia na Tume ya Jaji Kisanga ya mwaka 1998. Lakini mara
zote hizo mapendekezo hayo hayakukubaliwa.
Waasisi wa taifa letu, yaani Mwalimu Julius Nyerere,
aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Tanganyika wakati ule na Sheikh Abeid Amani
Karume, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar wakati ule,
waliamua kuchagua Muungano wa Serikali mbili tulionao sasa. Walitoa
sababu mbili kuu: “ni muundo unaoihakikishia Zanzibar kuwa
haimezwi na Tanganyika; na pia unaiepusha Tanganyika kubeba mzigo mkubwa
wa kugharamia Serikali ya Tanganyika na ile ya Muungano”.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Natambua kuwepo kwa rai ya kutaka Mwalimu Nyerere
asitumiwe katika mjadala huu. Nionavyo mimi ni vigumu kuacha kujadili
fikra za Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume katika jambo hili. Wao ndiyo
wa mwanzo kujadili na kukubaliana kuwa mfumo wa Serikali mbili ndiyo
bora kwa nchi yetu. Iweje leo tunapozungumzia kuubadili, mawazo yao yawe
hayafai kutumika au hata kuzungumzwa. Hivi hasa mawazo ya nani pekee
ndiyo bora zaidi kutumika? Tutakuwa hatuutendei haki mjadala huu na sisi
wenyewe tunaoshiriki katika mchakato huu. Rai yangu kwenu ni kuwa
mzitazame hoja zote kwa marefu na mapana yake ili mpime kama zipo sababu
za kuubadili muundo wa sasa wa Muungano wa Serikali mbili na kuleta wa
Serikali tatu. Na, kama zipo mabadiliko hayo yaweje! Lazima mfanye
uamuzi kwa utambuzi na hoja zenye mashiko. (you must make an informed decision).
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tume imetoa sababu mbili kubwa za kupendekeza muundo
wa Serikali tatu. Sababu ya kwanza ni kwamba ndiyo matakwa ya Watanzania
wengi kote Zanzibar na Tanzania Bara. Inaeleza kuwa idadi kubwa ya
Watanzania waliotoa maoni, yaani asilimia 60.2 wa kutoka Zanzibar wanaunga mkono muundo wa Serikali ya Mkataba, na asilimia61.3
wa kutoka Tanzania Bara wanaunga mkono muundo wa Serikali tatu. Sababu
ya pili ni kwamba muundo huo unatoa majawabu ya uhakika na endelevu kwa
changamoto za muundo wa sasa wa Serikali mbili zinazonung’unikiwa na
watu wa pande zetu mbili za Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Sababu hizi mbili kuu zilizotolewa na Tume zimezua
mjadala mkali katika jamii. Wapo wanaokubaliana na Tume na wapo
wasiokubaliana nayo. Wapo wanaosema Tume imesema kweli kwamba Watanzania
wengi wanaunga mkono muundo wa Serikali tatu, hivyo muundo wa Serikali
tatu hauepukiki. Ndiyo matakwa ya wengi hivyo msemo wa Kiswahili usemao
wengi wape uheshimiwe.
Lakini wapo wanaodai kuwa takwimu za Tume hazionyeshi
ukweli huo. Wanasema kuwa taarifa ya Tume imeonesha kuwa Watanzania
waliotoa maoni yao kwa Tume kwa mdomo na maandishi walikuwa 351,664. Kati yao ni wananchi 47,820 au sawa na asilimia 13.6 ndiyo waliokerwa na muundo wa Muungano hivyo wakauzungumzia. Wananchi 303,844 au sawa na asilimia 86.4 muundo wa Muungano kwao halikuwa tatizo, ndiyo maana hawakuuzungumzia kabisa. Wanahoji kuwa iweje leo asilimia 13.6 ya Watanzania wote waliotoa maoni wageuke kuwa ndiyo Watanzania walio wengi!
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Wanasema pia, kwamba mbona Taarifa ya Tume yenyewe, kuhusu takwimu (uk. 66 na 67), inaonesha kwamba kati ya hao watu 47,820 waliotoa maoni kuhusu Muungano, ni watu 17,280 tu ambao ni sawa na asilimia 37.2 ndiyo waliotaka muundo wa Serikali tatu, asilimia 29.8 walitaka Serikali mbili, asilimia 25.3 walipendekeza Serikali ya Mkataba na asilimia 7.7 walipendekeza Serikali moja. Hii hoja ya Watanzania wengi kutaka Serikali tatu msingi wake upi?
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Takwimu za Tume (uk. 57) zinaonyesha, vilevile kuwa Tume ilipokea maoni 772,211. Kati ya hayo asilimia 10.4 tu ndiyo yaliyozungumzia muundo wa Muungano na asilimia 88.6
hayakuzungumzia Muungano bali mambo mengine. Hivyo basi wanahoji pia
kwamba kama muundo wa Muungano ungekuwa ni jambo linalowakera Watanzania
wengi, lingedhihirika kwenye idadi ya watu waliotoa maoni na kwenye
idadi ya maoni yaliyotolewa. Yote hayo hayakujitokeza. Waliouzungumzia
Muungano walikuwa asilimia 13.6 tu ya watu wote waliotoa maoni na maoni yanayohusu Muungano yalikuwa asilimia 10.4 ya maoni yote. Hivyo basi, wanauliza “usahihi wa hoja ya Watanzania wengi kutaka Serikali tatu uko wapi?”
Changamoto za Muundo wa Serikali Mbili
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wajumbe;
Kama nilivyokwishagusia awali, sababu ya pili ambayo
Tume inatoa kuhusu kufaa kwa muundo wa Serikali tatu ni kwamba mfumo huu
unajibu changamoto nyingi za muundo wa Serikali mbili. Tume imeainisha
vizuri changamoto za muundo wa Serikali mbili. Kwa upande wa Zanzibar
wanalalamikia kile kinachoitwa Tanzania Bara kuvaa koti la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na hivyo kutumia mamlaka ya Serikali ya Muungano
kujinufaisha yenyewe. Fursa hiyo Zanzibar hainayo. Aidha, wanasema
mipaka na mamlaka ya Serikali ya Muungano kwa mambo ya Muungano, na kwa
mambo ya Tanzania Bara haijaainishwa vizuri ikaeleweka. Wazanzibari pia,
wanazungumzia mkanganyiko kuhusu ugawanaji wa mapato, na jinsi ya
kuchangia shughuli za Muungano baina ya Serikali ya Muungano na Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar. Vilevile, wanalalamikia Rais wa Zanzibar
kuondolewa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano. Aidha, kuna
malalamiko kuwa orodha ya mambo ya Muungano iliyoongezwa kutoka mambo 11 mwaka 1964 mpaka 22 mwaka 1992imepunguza uhuru wa Zanzibar kwa mambo yake ya ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa upande wa Tanzania Bara, Tume inaeleza kuwepo kwa
manung’uniko kuwa Muungano wa Serikali mbili umepoteza utambulisho wa
kihistoria wa Tanganyika na fursa ya watu wa upande wa Tanzania Bara
kutetea maslahi yao ndani ya Muungano. Wanasema Zanzibar sasa imekuwa
nchi huru; ina bendera yake, wimbo wake wa taifa na Serikali yake.
Aidha, wanasema Zanzibar imebadili Katiba na kujitambulisha kama nchi na
kuchukua madaraka ya Bunge la Muungano, kwa vile Sheria zinazotungwa na
Bunge lazima zipelekwe kwenye Baraza la Wawakilishi kupata kibali cha
kutumika Zanzibar. Wananchi wa Tanzania Bara pia wanalalamikia kutokuwa
na haki ya kumiliki ardhi Zanzibar wakati wenzao wa kutoka Zanzibar
wanayo haki hiyo Tanzania Bara. Na wao vilevile wananung’unikia
mkanganyiko kuhusu ugawaji wa mapato na jinsi ya kuchangia gharama za
uendeshaji wa shughuli za Muungano baina ya Serikali ya Muungano na
Serikali ya Zanzibar. Hizi ndizo baadhi ya changamoto ambazo Tume inaona
jawabu lake ili kuzitanzua ni kubadili muundo wa Muungano kuwa wa
Serikali tatu badala ya mbili za sasa.
Faida za Muundo wa Serikali Tatu
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tume ya Mabadiliko ya Katiba imefafanua kwamba mfumo
wa Serikali tatu utagawanya vizuri madaraka kati ya mamlaka tatu za
Muungano. Unawezesha Washirika wa Muungano kubaki na utambulisho wao wa
kihistoria na kiutamaduni na hivyo, utawezesha kuondoa hisia za Zanzibar
kumezwa na Muungano. Pia unawezesha kila upande wa Tanzania kuendesha
mambo yake yasiyo ya Muungano kadri wanavyoona inafaa. Vile vile unaweza
ukaleta ushindani wa kimaendeleo baina ya washirika na hivyo kusaidia
kukuza maendeleo ya nchi.
Faida za Muundo wa Serikali Mbili
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Pamoja na kuainisha changamoto za muundo wa Serikali
mbili na kupendekeza kuwa muundo wa Serikali tatu ndio utakaosaidia
kuzitatua, Tume haikuacha kutambua manufaa na mchango muhimu uliotolewa
na muundo wa Serikali mbili kwa nchi yetu. Tume inasema kuwa muundo wa
Serikali mbili unapunguza gharama za uendeshaji wa shughuli za umma.
Umesaidia kujenga uhusiano na ushirikiano mzuri katika 30nyanja
mbalimbali baina ya wananchi wa pande zetu mbili za Muungano. Umezuia
mkubwa kummeza mdogo; na umedumisha Muungano mpaka kuufikisha hapa ulipo
tangu kuasisiwa kwake takriban miaka 50 iliyopita (1964). Aidha,
umesaidia kudumisha amani, umoja na utulivu hapa nchini.
Changamoto za Muundo wa Serikali Tatu
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Pamoja na kuelezea ubora wa muundo wa Serikali tatu
kama jawabu kwa changamoto za Serikali mbili, Tume inakiri kuwa hata
muundo huu nao una changamoto zake. Kwanza kabisa, Taarifa ya Tume
inaeleza kuwa kutakuwa na gharama kubwa za uendeshaji wa shughuli za
umma. Mheshimiwa Jaji Joseph Warioba alitutoa hofu kuhusu gharama
ingawaje mwaka 1993, Mwalimu alikuwa na mawazo tofauti. Alisema kwamba: “watu …wanaodhani
kuwa gharama ya Serikali yo yote kati ya hizo ingekuwa ndogo,
(Waulizeni Wazanzibari) na wala gharama ya Serikali ya Shirikisho
isingekuwa ndogo hata bila gharama ya mambo yasiyo ya Shirikisho”.Ni matumaini yangu kwamba katika mjadala wenu mtajipa nafasi ya kulitafakari suala hili kubwa na nyeti.
Tume imesema pia kwamba, Muundo huu, unaweza kuibua
tatizo la uchangiaji wa gharama za uendeshaji wa shughuli za umma baina
ya nchi washirika. Vilevile, kuna uwezekano wa kuwepo sera zinazokinzana
au kutofautiana juu ya masuala ya msingi ya nchi na kuzua mgogoro kati
ya washirika wa Muungano na baina ya nchi washirika na Serikali ya
Muungano. Aidha, upo uwezekano mkubwa kwa muundo huu kuleta tofauti za
kimaendeleo baina ya pande mbili za Muungano kutokana na kila upande
kuwa na sera na mipango tofauti.
Tume pia imeelezea hatari ya muundo wa Serikali tatu kukuza hisia za utaifa (nationalistic feelings) kwa nchi washirika, hivyo kuweza kudhoofisha Muungano. Muundo huu pia unaweza kuleta misuguano (paralysis and deadklocs in decision making)
katika kufanya uamuzi juu ya masuala muhimu ya kitaifa. Changamoto hizo
si tu zinaweza kuwa tishio kwa ustawi wa Muungano bali pia hata uhai
wake. Kwa ajili hiyo kuchagua muundo wa Serikali tatu kuna maana ya
kufanya kazi ya ziada ya kuzikabili changamoto hizi ili zisiue Muungano
wenyewe. Changamoto ambazo si ndogo hata kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Wanaounga mkono muundo wa Serikali mbili wanasema
kuwa kwa mlolongo huu wa changamoto zilizoainishwa na Tume yenyewe,
unadhihirisha kuwa muundo wa Serikali tatu hautapunguza matatizo ya
Muungano wetu bali utayaongeza maradufu kuliko ilivyo sasa. Wanakiri
kuwepo kwa changamoto katika muundo wa sasa wa Muungano. Hata hivyo,
wanaamini zinaweza kushugulikiwa na kupatiwa ufumbuzi bila ya kuhitaji
kuwa na Serikali ya tatu. Wanatoa mifano kadhaa ya jinsi Serikali zetu
zilivyoshughulikia changamoto za Muungano katika kipindi cha uhai wake
na mafanikio yaliyopatikana.
Katika kushughulikia kero za Muungano, Serikali zetu
mbili ziliunda Tume ya Shelukindo mwaka 1992 na Kamati ya Pamoja ya
Serikali zetu mbili mwaka 1993. Mambo mengi yaliyoainishwa katika Tume
ya Shelukindo na Kamati ya Pamoja yameshughulikiwa na kupatiwa ufumbuzi.
Kwa upande wa kero zilizoelezwa kwenye Tume ya Shelukindo, ilipofikia
mwaka 2006 yalikuwa yamebakia mambo 13 kati ya 31. Kwa jumla, kwa kero zilizoibuliwa na Tume ya Shelukindo na Kamati ya Pamoja, hivi sasa yamesalia mambo sita tu. Kimsingi ni mambo yahusuyo maslahi ya kiuchumi na yote yapo katika hatua nzuri za kuyamaliza. Mambo hayo ni:
-
Mgawanyo wa mapato:
-
Hisa za SMZ zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki
-
Mgawanyo wa Mapato yatokanayo na faida ya Benki Kuu.
-
Utafutaji na uchimbaji mafuta na gesi asili.
-
Ushirikiano wa Zanzibar na taasisi za nje.
-
Ajira kwa watumishi wa Zanzibar katika taasisi za Muungano.
-
Usajili wa vyombo vya moto.
-
Tume ya Pamoja ya Fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Serikali zetu mbili zimeamua kwa dhati kutumia fursa
ya mchakato huu wa mabadiliko ya Katiba kuyamaliza yale yanayohitaji
kuingizwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mambo hayo
ni matatu yafuatayo:
-
Utafutaji na uchimbaji mafuta na gesi asili.
-
Ushirikiano wa Zanzibar na taasisi za nje.
-
Tume ya Pamoja ya Fedha.
Matatu mengine yatamalizwa kwa kutumia taratibu za
kiutawala. Hali kadhalika, katika kipindi cha mpito kinachopendekezwa na
Tume yaani 2015 – 2018 ni nafasi nzuri ya kushughulikia masuala yenye
migongano kati ya Katiba ya Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano. Mimi
naishi kwa matumaini na kwa vile tunayo dhamira njema ya kuimarisha
Muungano wetu, naamini tutaweza kuziondoa tofauti zilizopo.
Orodha ya Mambo ya Muungano
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kuhusu orodha ya mambo ya Muungano kuwa 22 badala ya 11
ya awali, napenda kuwahakikishia kuwa Serikali ya Muungano na Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar hazina kigugumizi wala upungufu wa dhamira ya
kisiasa ya kuyapunguza yale yanayopunguzika. Napenda kwanza kabisa,
ieleweke kuwa kilichoongeza orodha hiyo si hila za Serikali ya Muungano
kutaka kupunguza madaraka ya Zanzibar kwa mambo yake ya ndani. Na, wala
siyo udhaifu wa viongozi wa Zanzibar katika kutetea maslahi ya nchi yao.
La hasha.
Pili, naomba ieleweke kuwa, kila kilichoongezwa
katika Orodha ya Mambo ya Muungano kilikuwa na sababu inayoeleweka,
inayoelezeka na iliyokubalika na pande zote mbili za Muungano. Hakuna
hata jambo moja lililoingizwa kwenye Katiba kwa kificho. Taratibu
stahiki za kikatiba na kisheria zilifuatwa. Hoja ziliwasilishwa Bungeni
na kujadiliwa kwa uwazi na uamuzi ulifanywa na Bunge kwa kuzingatia
kanuni ya theluthi mbili ya kura za kila upande wa Muungano. Kumbukumbu
zipo katika Hansard za Bunge la Muungano, ambazo ziko wazi kwa kila mtu
anayetaka kuzisoma asome. Nashauri mkazisome ili mpate kujua ukweli na
undani wa kila kilichoongezwa na sababu za kufanya hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Nchi zetu mbili zilipoungana mwaka 1964 na kuzaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kulikuwa na mambo 11 kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano. Mambo hayo ni haya yafuatayo:
- Katiba ya Jamhuri ya Muungano,
- Mambo ya Nje,
- Ulinzi,
- Polisi,
- Hali ya Hatari,
- Uraia,
-
Uhamiaji,
-
Biashara ya nje na mikopo,
-
Utumishi katika Serikali ya Muungano,
-
Kodi ya Mapato, Kodi ya Makampuni, Ushuru wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa,
- Bandari, Mambo ya Anga, Posta na Simu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kati ya mwaka 1965 na 1992 mambo ya Muungano yaliongezeka kutoka 11 hadi kufikia 22,
kimsingi kutokana na mambo mbalimbali yaliyotokea nchini na kwenye
ukanda wetu wa Afrika Mashariki. Pande zetu mbili za Muungano
zilikubaliana kuwa mambo hayo yaongezwe katika Katiba na taratibu za
kisheria na Kikatiba zilifuatwa. Kwa idhini yako naomba nitoe maelezo
kwa ufupi kwa yale yaliyoongezwa na kitu kilichosababisha mabadiliko
hayo kufanywa.
-
Jambo la kwanza kuongezwa, yaani la 12 lilikuwa ni “sarafu, mabenki na fedha za kigeni”. Hii ilifanyika tarehe 10 Juni, 1965 kufuatia kuvunjika kwa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki (East African Currency Board) mwaka 1964. Kwa ajili hiyo, kila nchi mwanachama wa Jumuiya ililazimika kuwa na sarafu yake na mipango yake ya kusimamia mambo yake ya kibenki na fedha. Serikali zetu mbili zilikubaliana masuala hayo yashughulikiwe na Serikali ya Muungano na Muswada husika wa Bunge uliidhinishwa kuwa Sheria na Mzee Abeid Amani Karume aliyekuwa akikaimu Urais tarehe 10 Juni, 1965.
- Tarehe 11 Agosti, 1967 yaliongezwa mambo yafuatayo kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano:-
- Leseni za Viwanda na Takwimu, (Jambo la 13)
- Elimu ya Juu, (Jambo la 14)
-
Jambo la 15 lilikuwa ni mambo yote yaliyokuwa kwenye Nyongeza ya 10 ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Nyongeza hiyo ilikuwa na mambo 27 ambayo Serikali ya Muungano ilipewa jukumu la uratibu. Mambo hayo ni pamoja na Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki, Utabiri wa Hali ya Hewa, Utafiti, Vipimo na Mizani, Huduma ya Usafiri wa Reli, Barabara, Usafiri wa Majini na kadhalika.
-
Tarehe 22 Julai, 1968 “rasilimali ya mafuta, petroli na gesi asilia” iliongezwa kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano na kuwa jambo la 16. Kimsingi Serikali ya Muungano ilipewa jukumu la kuagiza mafuta ya petroli na gesi asilia kwa ajili ya nchi nzima. Baada ya kupanga upya Orodha ya Mambo ya Muungano, suala la rasilimali ya mafuta likawa la 15.
-
Tarehe 22 Novemba, 1973 Baraza la Mitihani la Taifa liliongezwa na kuwa jambo la 16. Hii ilifuatia kuvunjika kwa Baraza la Mitihani la Afrika Mashariki mwaka 1971 na hivyo nchi yetu kulazimika kuunda Baraza la Mitihani la Taifa mwaka 1973.
-
Mwaka 1984 yalipofanyika mabadiliko makubwa katika Katiba ya mwaka 1977, Orodha ya Mambo ya Muungano ilipangwa upya. Mambo yaliyokuwemo kwenye Nyongeza ya 10 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuorodheshwa kama Jambo la 15 katika Orodha ya Mambo ya Muungano yalipunguzwa na kubaki matano. Mambo hayo yalipewa namba kama ifatavyo:- Usafirishaji wa Anga kuwa Jambo la 17, Utafiti kuwa la 18, Utabiri wa Hali ya Hewa kuwa la 19 na Takwimu kuwa la 20 na Mahakama ya Rufani ya Tanzania ikawa jambo la 21.
-
Tarehe 17 Mei, 1992 likaongezwa jambo la “Uandikishaji wa Vyama vya Siasa” na kuwa jambo la 22. Hii ilifuatia kuanzishwa kwa Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa na hasa uamuzi kuwa vyama vitakuwa vya kitaifa.
Bila ya shaka maelezo haya yatasaidia kuelezea nini
kimeongezwa na mazingira ya kuongezwa kwake ni yepi. Kulikuwepo na
sababu za msingi na wala siyo hila ya namna yo yote ile iliyofanywa na
mtu ye yote mwenye nia mbaya na Zanzibar. Kama tulivyoona mambo mengi
yalihusu kilichokuwa kinatokea ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kila yalipotokea mabadiliko katika uendeshaji wa shughuli za Jumuiya ya
Afrika Mashariki, huduma zilizokuwa zikitolewa na Jumuiya zilikabidhiwa
Serikali ya Muungano kubeba kwa sababu ya uwezo wake mkubwa wa kiuchumi.
Yale yaliyokuwa yanagusa sehemu zetu mbili za Muungano yaliingizwa
katika Orodha ya Mambo ya Muungano. Mengineyo yaliachiwa kila upande
kushughulikia ilivyoona inafaa. Kwa maana hii basi, mambo ambayo
yalitokana na uamuzi wetu wenyewe ni mawili tu. Mambo hayo ni rasimali
ya mafuta na gesi asilia (1968), na uandikishaji wa vyama vya siasa
(1992).
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Ni msimamo wa Serikali zetu mbili, tangu mwanzo mpaka
leo kwamba, iwapo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeshajenga uwezo
wake wa kufanya baadhi ya mambo katika Orodha ya Mambo ya Muungano ipewe
uhuru wa kufanya hivyo. Lililo muhimu ni kuwa zisiondolewe tunu zenyewe
za Muungano wetu. Ndiyo maana, mambo kama vile bandari, takwimu, kodi
ya mapato, leseni za biashara, utafiti na mengineyo, yanasimamiwa na
kuendeshwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na kuwemo kwenye
Orodha ya Mambo ya Muungano. Imekuwa hivyo kwa miaka kadhaa sasa na
imethibitika kuwa Zanzibar inayamudu. Ni makusudio yetu kutumia fursa ya
mchakato huu sasa kuyaondoa rasmi mambo hayo na mengineyo
tutakayokubaliana kutoka kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano.
Rasilimali ya Mafuta na Gesi Asilia
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa ajili hiyo tumekubaliana kuliondoa suala la
rasilimali ya mafuta na gesi asilia lisiwe jambo la Muungano. Jambo hili
tulishakubaliana tangu wakati wa Rais Amani Abeid Karume tuliondoe na
hata alipokuja Rais Shein msimamo haukubadilika. Kilichotuchelewesha
kutekeleza ni kuibuka kwa fikra za kuwa na mchakato huu wa Katiba mpya.
Tuliona kuwasilisha Bungeni Muswada wa Sheria wa kuondoa jambo hili
katikati ya mchakato huu, ingeweza kuzua matatizo yasiyokuwa ya lazima.
Tungeulizwa haraka ni ya nini tungeweza kukosa majibu.
Hatimaye wakati wake wa kulimaliza suala hili sasa
umefika. Misemo ya wahenga ya “subira yavuta heri” na “kawia ufike”
imetuongoza vyema tumefika mahali tunaweza kufanya hivyo. Zipo sababu
mbili zilizotushawishi kuamua kuitoa rasilimali hii kwenye Orodha ya
Mambo ya Muungano. Kwanza kwamba, siku hizi Serikali haiagizi mafuta.
Kazi hiyo hufanywa na makampuni binafsi. Pili, kwamba, rasilimali ya
mafuta na gesi yakipatikana Zanzibar ni suala la kiuchumi ambalo lipo
kwenye mamlaka ya Zanzibar kama ilivyo karafuu, hiliki, mwani na
kadhalika. Au kama ilivyo dhahabu, gesi, pamba, kahawa na kadhalika kwa
upande wa Tanzania Bara. Hivyo, Zanzibar iachwe kumiliki rasilimali yake
ya kiuchumi.
Zanzibar na Ushirikiano wa Kimataifa
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Jambo lingine muhimu ambalo Serikali zetu mbili
zimelizungumza na kukubaliana tulitafutie ufumbuzi ni kuhusu Zanzibar
kupata fursa ya kujiunga na mashirika ya kimataifa, kukopa na kupata
misaada kutoka nchi za nje bila kizuizi. Kwa sasa fursa hiyo ina vikwazo
vya namna mbalimbali. Ni ukweli usiopingika kuwa jambo hili limechangia
kwa kiasi kikubwa kujenga hisia hasi kuhusu Muungano kwa upande wa
Zanzibar. Aidha, limechangia sana kuchafua hali ya hewa ya kisiasa
Zanzibar kwa nyakati mbalimbali. Hata zile kauli kwamba Tanzania Bara
imejificha kwenye koti la Serikali ya Muungano, na kutaka itoke ionekane
ili iache kunufaika isivyostahili, zinazochangiwa sana na mazingira
haya iliyonayo Zanzibar. Serikali zetu mbili zinaamini kuwa mambo haya
yakipatiwa ufumbuzi tutakuwa tumeondoa kizingiti kikubwa katika ustawi
wa Muungano wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tumekubaliana kuwa, tutumie fursa za
mchakato huu kuyamaliza mambo haya yaishe! Bahati nzuri dhana iliyopo
katika Ibara ya 65(2) ya Rasimu inatoa jawabu mwafaka kwa tatizo hili.
Tukikubaliana, itaipa Zanzibar “uwezo na uhuru wa kuanzisha uhusiano na
ushirikiano na jumuiya au taasisi yo yote ya kikanda na kimataifa kwa
mambo yaliyo chini ya mamlaka yake kwa mujibu wa Katiba ya nchi” bila
kizuizi. Ni maoni ya Serikali zetu mbili kuwa fursa hiyo inaweza
kutolewa kwa Zanzibar bila ya kulazimika kuwa na muundo wa Serikali
tatu. Hatuuoni ulazima huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa maoni yangu kitu kingine muhimu cha kufanya ni
kuongeza msukumo, utakaohakikisha kuwa Tume ya Pamoja ya Fedha inatimiza
ipasavyo majukumu yake. Wanaohusika na utekelezaji wa maamuzi yake
wabanwe ipasavyo kutimiza wajibu wao. Iwekwe mifumo na masharti katika
sheria au Katiba ya kuwabana watekelezaji kwa ajili hiyo. Hali kadhalika
ihakikishwe kuwa, Akaunti ya Pamoja inaanzishwa bila ajizi na kutumika
na pande zote. Aidha, mfumo wa mawasiliano na ushirikiano baina ya
Serikali zetu mbili yaani Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Muungano na
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, upewe nguvu ya kisheria na kama hapana
budi upewe nguvu ya Kikatiba. Tukifanya hivyo tutafanikiwa kuyaweka
mambo yote sawa hata bila ya kuhitaji kuunda Serikali ya tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Waheshimiwa Wajumbe;
Katika mjadala kuhusu mapendekezo ya kuwa na muundo
wa Muungano wenye Serikali tatu, wananchi wametoa maoni na mapendekezo
mengi mazuri kuhusu changamoto za Serikali tatu zilizoainishwa na Tume
na namna ya kuzitatua. Tena yapo maoni ya watu wanaopenda muundo wa
Serikali tatu na wasiopenda muundo wa Serikali tatu. Nawaomba
myatafakari kwa uzito unaostahili. Yapo mambo muhimu ya kuyatafutia
ufumbuzi. Kwanza, kwa mfano ni ile hoja kwamba Serikali ya Muungano
inayopendekezwa haikujengeka kwenye msingi imara. Haina nguvu yake
yenyewe za kusimama. Inategemea mno ihsani ya nchi washirika. Kwa sababu
hiyo inaweza kuanguka wakati wowote, na Muungano kusambaratika, iwapo
itakosa ihsani ya nchi washirika. Tena inaweza kuwa hivyo hata kama ni
mmoja wa washirika amefanya hivyo.
Pili, kwamba, haielekei Serikali hiyo ina chanzo cha
uhakika cha mapato ya kuiwezesha kusimama yenyewe na kutekeleza majukumu
yake. Ushuru wa bidhaa unaopendekezwa unatiliwa shaka kuwa
hautatosheleza mahitaji. Pia, kwamba, hakuna uhakika wa fedha hizo
kupatikana kwa vile, Serikali ya Muungano haina chombo chake chenyewe
cha kukusanya mapato hayo. Itategemea vyombo vya nchi washirika
kuikusanyia na kuipelekea. Kuna hatari ya shughuli za Serikali ya
Muungano kusimama wakati wo wote au hata kusimama kabisa kwa sababu ya
nchi washirika kuchelewa au kushindwa kuwasilisha makusanyo ya kutoka
kwao.
Bahati mbaya Serikali ya Muungano haina uwezo wala
nyenzo za kuhakikisha kuwa mapato yake yanawasilishwa. Serikali hiyo
haina mamlaka ya kuzibana nchi washirika kuwasilisha au kuziwajibisha
zisipofanya hivyo. Katika mazingira hayo ni rahisi kwa Serikali ya
Muungano kukwama na kushindwa kutekeleza majukumu yake. Huu ni muundo
ambao inakuwa ni rahisi sana kwa Muungano kuvunjika.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Katika Rasimu ya Katiba, Serikali ya Muungano inapewa
fursa ya kukopa kama chanzo cha kujipatia mapato ya kuendesha shughuli
zake. Lakini, kwa sababu ya kukosa rasilimali zake yenyewe, huenda ikawa
vigumu kwa Serikali hiyo kukopesheka. Kwa jumla hii ni Serikali ambayo
ukuu wake hauna nguvu iliyo thabiti, na watu wengine wanaona kama vile
ukuu huo haupo kabisa. Akitokea kiongozi ye yote wa nchi washirika
akatunisha misuli dhidi ya Rais wa Muungano au kupinga maamuzi ya
Serikali au chombo cha Muungano, Rais na Serikali yake watakuwa hawana
lo lote la kufanya. Kwa kweli uhai wa Muungano katika muundo wa Serikali
tatu ni wa mashaka makubwa.
Hofu hizi kuhusu udhaifu wa Serikali ya Muungano
chini ya mfumo wa Serikali tatu unaopendekezwa, zinawasumbua hata wale
wanaopendelea mfumo wa Serikali tatu kuwepo. Wao wangependa iwepo
Serikali ya Muungano yenye nguvu na inayoweza kusimama yenyewe kwa
kujitegemea. Wanaona kilichopendekezwa hakitoi matumaini hayo. Hii ina
maana kuwa lazima mawazo bora zaidi yatolewe ili kupata Serikali ya tatu
yenye ukuu unaoonekana na inayoweza kusimama yenyewe bila kuwa tegemezi
na egemezi kwa nchi washirika. Pia inaweza kuwa nguzo ya kutegemewa na
nchi washirika. Bila ya shaka Bunge hili likiamua tufuate mfumo huo
linaweza kuonyesha njia ya kuondoa hofu hizo. Kwa waumini wa Serikali
mbili wanaona kuwa huu ni uthibitisho wa ubora wa muundo wa Serikali
mbili.
Changamoto za Hisia za Utaifa
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Katika kuainisha changamoto za muundo wa Serikali
tatu, Tume ya Mabadiliko ya Katiba imeyataja mambo mengine mawili
makubwa ambayo ningependa Waheshimiwa Wajumbe muyape tafakuri stahiki.
Mambo hayo ni mosi, misuguano na mikwamo (deadlocks and paralysis) katika kujadili na kufanya uamuzi kuhusu mambo muhimu ya Muungano. Na pili, ni kuibuka kwa hisia za utaifa (nationalistic sentiments)
wa zamani kwa nchi washirika. Nawaomba myatafakari kwa makini sana
mambo haya, kwa sababu ya uwezo wake mkubwa wa kuhatarisha siyo tu
ustawi na uhai wa Muungano, bali hata usalama wa raia na mali zao. Naona
hata Tume haikuweza kupata ufumbuzi ulio mwafaka kabisa kwa changamoto
hizi. Bila ya shaka katika mijadala yenu Waheshimiwa Wajumbe mnaweza
kusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Ni lazima lifanyike kila linalowezekana kuhakikisha
kuwa maamuzi hayakwami kwani yakikwama maana yake shughuli za Muungano
zitakuwa zimekwama. Kama hazitakwamuliwa kwa wakati ustawi wa Muungano
utaathirika. Ikishindikana kabisa kupatikana ufumbuzi Muungano unaweza
kuvunjika. Kuibuka na kukua kwa hisia za utaifa (nationalistic feelings)
kwa nchi washirika, yaani Utanganyika na Uzanzibari ni tishio kubwa
sana kwa uhai wa Muungano. Hebu fikiria, watu walioishi pamoja kidugu na
kwa kushirikiana, kama watu wamoja na raia wa nchi moja yaani
Watanzania kwa miaka 50, kuja kujikuta uhusiano wao kuwa ni kati ya
Watanganyika na Wazanzibari na siyo kati ya Watanznaia. Kwa mujibu wa
sensa iliyopita takriban asilimia 90 ya Watanzania waliopo sasa
wamezaliwa baada ya mwaka 1964. Nchi wanayoijua ni Tanzania. Litakuwa ni
jambo lenye mshtuko mkubwa na athari zisizoweza kutabirika, watu hao
watakapojikuta ni wageni wanaotakiwa kutengenezewa utaratibu maalum wa
kusafiri na kuishi wakiwa upande wa Muungano ambao siyo kwao kwa asili.
Wanakuwa wageni na fursa walizokuwa wanazipata waendapo popote haiwi
rahisi tena kuzipata.
Katika mazingira hayo ni rahisi sana chuki
kupandikizwa na watu waliokuwa ndugu mara moja watajikuta maadui. Aidha,
watu wanaweza kujikuta wakilazimika kurudi kwao kwa asili ama kwa
kufukuzwa au kwa sababu ya mazingira kuwa magumu kiasi cha kuona bora
waondoke. Watu hao wanaweza kulazimika kuondoka huku wakiacha nyuma kila
kitu walichokichuma maishani.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Changamoto hizi kubwa mbili za mfumo wa Serikali tatu
ambazo Tume imeziona, ni za kweli. Si mambo ya kufikirika. Yale
yaliyowakuta watu wenye asili ya Tanzania Bara ya kuchomewa moto
biashara zao Zanzibar mwaka 2012 na watu wenye hisia kali za Uzanzibari,
na kuwataka watu wa Bara waondoke Zanzibar, huenda yakawa madogo.
Matukio ya namna hii yanaweza kutokea pande zote mbili na kusababisha
maafa makubwa. Itaanza baina ya watu, baadaye itakuwa baina ya Serikali
zetu mbili na kuzifikisha nchi zetu mbili zilizokuwa ndugu na rafiki,
kwa nusu karne, ghafla kuwa maadui wasioombana chumvi na wasiotakiana
heri. Umoja wetu utatetereka na Muungano wetu unaweza kuvunjika. Kwa
nini tufike huko?
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Sisi viongozi tuliopewa dhamana ya kuamua kwa niaba
ya wananchi wetu, hatuna budi kuyapima mambo haya kwa umakini mkubwa ili
tufanye uamuzi ulio sahihi. Tusije tukajutia uamuzi wetu tutakapoona
watu wanafukuzana, wanauana na mali zao kuporwa. Na, tukifikia hatua
hiyo Muungano kusambaratika halitakuwa jambo la ajabu.
Kwa kweli, unapoyatafakari haya, ni rahisi kuelewa
kwa nini wazee wetu waasisi waliamua walivyoamua. Waliona mbali.
Tusipuuze fikra zao na maono yao. Kuna hatari ya nchi yetu na watu wake
kupoteza kila kitu tulichokijenga kwa miaka 50. Badala ya kujenga
tunaweza kujikuta tumebomoa hata msingi katika nchi washirika. Baba wa
Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1993 alituasa kuhusu hatari hiyo: “Hamuwezi kutenda dhambi kubwa namna hiyo bila adhabu… na adhabu nyingine zimo mle mle ndani ya kitendo hazisubiri.”
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Siku moja kiongozi mmoja wa juu wa madhehebu ya dini nchini aliniuliza: “Hivi
Serikali mbili zikiwa na matatizo jawabu ni kuongeza ya tatu? Si
matatizo ndiyo yatazidi? Je, matatizo yakizielemea hizo Serikali tatu si
kila mtu atachukua njia yake? Mtakuwa mmepoteza kila kitu. Mimi
nawashauri msichoke kutafuta majawabu kwa matatizo ya hizi mbili! Huko
mnakotaka kwenda kuna hatari nyingi”.
Pengine na ushauri huu wa mtu wa Mungu nao ni vyema kuupa nafasi na kuutafakari.
Kazi Yenu Kubwa
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Mambo ya kuyasemea ni mengi mno lakini kwa sababu ya
ufinyu wa muda, nisingeweza kuyazungumzia yote. Naamini, mtayaona katika
kuipitia Rasimu na kwenye majadiliano yenu. Napenda kusisitiza kwenu
kuwa kazi iliyo mbele yenu ni kubwa sana. Ni kubwa kwa maana mbili.
Kwanza, jukumu lenyewe la kutunga Katiba ya nchi ni zito sana. Taswira
ya nchi yetu itakuwaje na itaendeshwa vipi kwa miaka mingi ijayo iko
mikononi mwenu. Ipeni nchi yetu hatima njema. Pili, ni kubwa kwa maana
ya uzito wa mambo ya kujadili na kuyafanyia uamuzi. Kwa ajili hiyo, ni
muhimu sana kuisoma Rasimu na Taarifa ya Tume kwa makini na kuzielewa.
Jipeni muda wa kutafakari kila neno, kila sentensi, na kila dhana ili
muweze kufanya uamuzi ulio sahihi. Mkifanya hayo mtakuwa mmeisaidia nchi
yetu na Watanzania wote kupata Katiba nzuri.
Nimefarijika sana kusikia kuwa mtajigawa kwenye
Kamati 12 wakati wa kujadili Rasimu. Huu ni utaratibu mzuri kwani mkiwa
katika vikundi vya watu wachache, mtakuwa na mijadala ya kina zaidi.
Watu wote wanaweza kupata fursa ya kutoa maoni yao, kwa kila kifungu na
kila jambo linaloibuliwa na kuzungumzwa. Kwa kufanya hivyo, mtatimiza
kwa ukamilifu jukumu lenu la kutunga Katiba. Wote mtakuwa mmeshiriki
kujadili kila sura na vipengele vyake vyote. Mkimaliza kazi yenu
mtapokea kwa haki sifa nzuri kama Katiba itakuwa nzuri, au lawama
stahiki iwapo itakuwa kinyume chake.
Pongezi kwa Mwenyekiti wa Muda
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Nitakuwa mwizi wa fadhila kama nitamaliza hotuba
yangu bila ya kutambua kazi nzuri iliyofanywa na Mheshimiwa Pandu Ameir
Kificho, Spika wa Baraza la Wawakilishi, alipokuwa Mwenyekiti wa Muda wa
Bunge hili. Kazi yake haikuwa rahisi hata kidogo, lakini kwa umahiri na
ustadi mkubwa ameweza kufanikisha mambo kwa kiasi ambacho anastahili
pongezi zetu sote. Anastahili pongezi kwa sababu yeye aliendesha Bunge
hili bila ya kuwepo kwa kanuni. Tatizo hili hatakuwa nalo Mwenyekiti wa
Kudumu kaka yangu Mheshimiwa Samuel Sitta.
Napenda pia kuwapongeza Waheshimiwa Wajumbe wa Bunge
Maalum la Katiba kwa hatua mliyofikia. Hata hivyo, mmechukua muda mwingi
katika hatua ya awali hivyo hamna budi kuongeza kasi. Naomba
niwakumbushe kuwa mijadala yenu hii inafuatiliwa kwa karibu sana na
Watanzania. Wamewekeza sana matarajio yao kwenu. Hamna budi, haiba na
taswira ya uongozi muionyeshe wakati wote wa kuendesha mijadala yenu kwa
lugha na vitendo vyenu. Wakati wa semina na mjadala wa kupitisha Kanuni
za Bunge hili, baadhi ya wananchi wamekwazika sana na mwenendo wa
baadhi ya Wajumbe. Hawakutegemea kuyaona matendo waliyoyaona mkifanya na
kusikia maneno waliyoyasikia kutoka kwenye vinywa vya baadhi yenu.
Ni matumaini yangu na ya Watanzania wote kuwa hali
ile haitajirudia tena katika awamu hii. Tusiwafikishe mahali Watanzania
wakakata tamaa na Wajumbe wao au na hata chombo hiki muhimu sana kwa
mustakabali wao na wa nchi yao. Tutoe hoja badala ya kupiga kelele (argue don’t shout) au
kuzomea. Hakuna haja ya kutumia lugha isiyokuwa ya staha katika
kujieleza. Hakuna haja ya kukingiana ngumi, kutishiana hili na lile au
hata kugombana. Ni utovu wa uungwana usiotegemewa kutoka kwenu.
Tusiwaangushe wananchi wa Tanzania wanaotutegemea sana.
Wekeni Maslahi ya Taifa Mbele
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Ombi langu la mwisho kwenu ni kuwasihi kuwa wakati
wote muongozwe na kujali maslahi mapana ya nchi yetu na watu wake badala
ya kujali maslahi yenu binafsi au ya makundi yenu. Naomba kaulimbiu
yenu iwe “Tanzania Kwanza”. Najua kila mmoja wenu amekuja na
maoni yake au atakuwa nayo kwa kila jambo litakalojadiliwa. Wengine
wamepewa misimamo na vyama vyao au makundi yao. Si jambo baya na ni
hatua muhimu ya kuleta mafanikio, kama misimamo hiyo na mawazo hayo ni
ya kujenga.
Hata hivyo, mnachotegemewa kufanya ni kuwa tayari
kuwianisha na kuunganisha mawazo yenu mazuri na ya wenzenu, ili kupata
msimamo wa pamoja na uamuzi wa pamoja ulio bora. Kwa sababu hiyo, hamna
budi kuwa tayari kusikiliza mawazo ya wengine, hata kama ni tofauti na
yenu mliyokuja nayo. Tafuteni kilicho chema kwa yale yanayosemwa na watu
wengine hata kama ni watu usiokubaliana nao au huwapendi au hampendani.
Kunaweza kuwepo kitu chenye manufaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wajumbe;
Nawaomba muwe hodari wa kushawishi badala ya
kulazimisha. Mkifanya hivyo hamtalazimika kutumia muda mwingi wa kula
njama za namna ya kuwazidi maarifa wale mnaotofautiana nao kwa mawazo.
Lazima pia mtafute namna ya kushirikiana na kuwasiliana na makundi
mengine. Msitafute kushindana, hili ni jambo ambalo lazima wote mtoke
hapa mkiwa washindi. Yaani lazima Watanzania wote washinde kwani wao
ndiyo wenye Katiba yao. Nawapongeza viongozi wa vyama vya siasa na asasi
mbalimbali kwa kutambua na kuthamini umuhimu wa kuwa na taratibu za
mawasiliano, mashauriano na ushirikiano. Daima muwe watu wa kutafuta
maridhiano. Mmefanya vizuri katika hatua ya awali. Mmejiwekea taratibu
nzuri za kufanya hayo, tafadhalini zitumieni. Jengeni madaraja imara
zaidi katika awamu hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Naomba nimalize kwa kuwaomba Watanzania wote
tukiongozwa na viongozi wetu wa dini tumuombe Mola wetu ajalie rehema
zake ili mchakato wa kutunga Katiba uende salama. Aliongoze Bunge hili
na Wajumbe wake waweze kufanya uamuzi ulio sahihi na wenye manufaa kwa
taifa letu kwa kila watakaloliamua.
Baada ya kusema maneno yangu mengi hayo, nirudie
kukushukuru Mheshimiwa Mwenyekiti kwa kunipa fursa hii adhimu ya
kulihutubia Bunge Maalum la Katiba. Nawatakieni kila la heri na
mafanikio mema. Katiba Mpya Inawezekana,Timiza Wajibu Wako.
CHANZO:ZANZIBAR ISLAMIC NEWS BLOG
CHANZO:ZANZIBAR ISLAMIC NEWS BLOG
No comments:
Post a Comment