Afafanua utata ulioibuliwa katika taarifa yake mbele ya Bunge la Katiba.
Dar es Salaam. Wakati Ikulu ikitangaza kwamba Rais Jakaya Kikwete
amevunja Tume ya Mabadiliko ya Katiba, tume hiyo imetoa ufafanuzi wa
baadhi ya maeneo ya Rasimu ya Katiba.
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta (kulia) akiongoza kikao cha kwanza cha Kamati ya Uongozi ya Bunge hilo, mjini Dodoma jana.
Taarifa ya Ikulu iliyotolewa jana, ilieleza kuwa Tume ya Jaji Joseph
Warioba ilivunjwa tangu Machi 19, ikiwa ni siku moja baada ya
kuwasilisha Rasimu ya Katiba bungeni mjini Dodoma.
Wakati taarifa ya Tume ya Warioba ilitolewa jana jioni, Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Rais, Ikulu ilikuwa imeshatoa taarifa ya kuvunja tume
hiyo mapema jana ikieleza kuwa shughuli za tume hiyo zilikoma tangu
Jumatano iliyopita.
“Kwa mujibu wa kifungu cha 31 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Rais
wa Jamhuri ya Muungano alivunja rasmi Tume ya Mabadiliko ya Katiba
tarehe 19 Machi, 2014 kwa Tangazo la Serikali Na.81 la tarehe 21 Machi,
2014,” ilisema taarifa hiyo ya Ikulu.
Hata hivyo, Jaji Warioba aliliambia gazeti hili jana kuwa hadi
wanakutana juzi kwenye kikao cha mwisho cha tathmini walikuwa
hawajapokea barua ya kuvunjwa kwa tume yake.
“Barua ya Ikulu tumeipokea leo. Tulikuwa hatuna taarifa kwamba tume yetu
imevunjwa hadi tulipopokea barua leo (jana). Tulifanya kikao chetu cha
mwisho cha tathmini jana (juzi),” alisema Warioba alipozungumza na
Mwananchi jana jioni.
Warioba pia alithibitisha kwamba taarifa ya ufafanuzi (imechapishwa ukurasa wa 37) ni ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Taarifa hiyo ya Tume ya Warioba imetaja baadhi ya sababu za kupendekezwa
kwa muundo wa serikali tatu kuwa, ni pamoja na Serikali ya Muungano
kutokuwa tena na nguvu upande wa Zanzibar na Rais kupokwa baadhi ya
madaraka aliyopewa kikatiba.
Ufafanuzi wa Tume
Taarifa hiyo ya tume ilisema: “Waasisi walituachia mambo 21 (ukiacha
usajili wa vyama) kwenye orodha ya Muungano. Katika kipindi cha miaka
ishirini iliyopita yamepunguzwa. Mambo yote yaliwekwa kwa utaratibu
uliowekwa na Katiba lakini yameondolewa kinyume na Katiba.”
Iliongeza: “Sehemu zote mbili ziliamua kuachia baadhi ya mambo yake kuwa
chini ya Serikali ya Muungano, sasa sehemu moja inaondoa mambo yake.
Kwa hiyo Serikali ya Muungano itakuwa inashughulikia zaidi mambo ya
upande mmoja.”
Kasoro nyingine iliyotajwa na tume hiyo ni hatua ya waasisi wa Muungano
kuwa waliacha Bunge lenye madaraka nchi nzima, lakini sasa ni lazima
sheria linazotunga zipate idhini ya Baraza la Wawakilishi kwa upande wa
Zanzibar.
“Waasisi waliacha Rais akiwa na madaraka kamili. Madaraka hayo
yamepunguzwa bila kufuata utaratibu wa Katiba. Waasisi walituachia
Mahakama ya Rufani yenye madaraka kamili. Madaraka haya yamepunguzwa.
Waasisi waliunganisha nchi mbili ikawa moja. Sasa tunazo nchi mbili,”
ilisema taarifa hiyo na kuongeza:
“Hii ndiyo inafanya wananchi wa Tanzania Bara waamini Zanzibar ni huru
katika mambo yao. Wanaona ina mamlaka kamili kushughulikia mambo yake
na imechukua rasilimali zake. S
erikali ya Muungano imebaki na mamlaka na rasilimali za Tanzania Bara.”
Taarifa hiyo ilisema wakati wabunge wa Zanzibar wanashiriki kuamua mambo
ya Tanzania Bara, wabunge wa Tanzania Bara hawana nafasi ya kushiriki
katika kuamua mambo ya Zanzibar.
Tume hiyo ilisema ilikuwa vigumu kwa Zanzibar kurudi kwa hiyari kwenye
hali ya awali, ikiwa ni pamoja na kufuta kipengele cha nchi mbili kwenye
Katiba yake, hivyo waliamua kupendekeza mfumo wa serikali tatu kama
hatua ya kuzingatia malalamiko ya Tanzania Bara.
Tume iliona kwamba pamoja na mambo haya kufanywa kinyume na Katiba ya
Muungano, hali ibaki hivyo hivyo. Lakini kwa kufanya hivyo basi nayo
yasipuuzwe. Hivyo Tume nayo ikapendekeza Serikali ya Tanganyika iundwe.
Hali ilivyo
Tume hiyo imevunjwa huku kukiwa na mjadala mkali kuhusu hotuba ya Jaji
Warioba katika Bunge Maalumu pamoja na ile ya Rais Kikwete aliyoitoa
wakati akizindua Bunge hilo, Machi 21, mwaka huu.
Kutokana na hotuba hizo kukinzana, hasa kuhusu aina ya muundo wa
Muungano unaotakiwa, baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu walipendekeza
Jaji Warioba apewe fursa ya kuitwa bungeni kutoa ufafanuzi wa masuala
mbalimbali na pengine kujibu baadhi ya hoja zilizoibuliwa na Rais
Kikwete.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliundwa kwa mujibu wa kifungu cha 5 na 6
cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 kwa Tangazo la Serikali
Na.110 la 2012.
Wajumbe wake 30 waliteuliwa na Rais Kikwete kwa kushirikiana na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.
CHANZO:Mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment